Monday, June 24, 2013

SIWEZI KUSAHAU KISA HIKI

Ilikuwa mwezi wa 10 mwaka 2005 nilipojiunga na chuo kikuu cha Dar es Salaam kusoma shahada yangu ya kwanza ya Sayansi katika Uhandisi wa Kompyuta na Teknolojia ya Habari (Bsc. in Computer Engineering and IT). Mimi pamoja na vijana wenzangu tuliotoka kwenye familia zilizo na uwezo wa kawaida sana na ambao ki msingi ni familia za wakulima za huko vijijini hapa nchini tulikuwa na wakati mgumu kidogo kuendana na mazingira ya chuo kikuu na jiji la Dar es Salaam kwa ujumla. Wanafunzi wa kiume waliochaguliwa kusoma shahada hii wengi wetu tulipewa vyumba vya malazi (accommodation) katika ghorofa moja pale kampasi kuu (main campus) jengo namba 2 (hall 2) ghorofa ya 7 na 8 (7th and 8th floor). Baada ya kujiunga na chuo tulitegemea kuanza kupatiwa sehemu ya mkopo kwa wanafunzi kwaajili ya chakula, malazi na vifaa vya kusomea (meal, accommodation and stationary) wakati huo ikiwa ni asilimia mia (100%). Badala yake mkopo huo ulichelewa kwa zaidi ya wiki mbili na kusababisha adha kubwa kwa wanafunzi pale chuoni. Ilitulazimu kuanza kuwasiliana na ndugu jamaa na marafiki ili kupata walau vijisenti vya kujikimu. Bahati mbaya mkopo uliendelea kuchelewa hadi kufukia kiasi wanafunzi kuanzisha mgomo mkubwa ukiongozwa na Raisi wa serikali ya wanafunzi (DARUSO) na waziri mkuu wake, wakati huo Mwita Waitara na John Mrema. Sikuchache kabla ya mgomo huo sisi tulianzisha mtindo maarufu wa KUPUNGUZA KULA KUBANA MATUMIZI uliokuwa ukiitwa "KUPIGA DESH ama PASI NDEFU", siku moja nilijikuta nikipiga pasi ndefu sana hadi nikadhoofika, nikaacha vipindi darasani na kwenda chumbani HALL II kulala, kwa bahati mbaya ama nzuri mwenye funguo wa chumba hakuacha funguo mahali ambapo huwa tunaweka, ikanilazimu kwenda kulala chumba cha jirani kwa rafiki yangu Musa Chibali Semwenda niliyekuwa nikisoma naye darasa moja pamoja na Edgar Tenga, Beatus FK, Linda Joseph, Irene Dubi Makundi, Paul G Mandu, William Nzunda, Hellen Maziku, Irene Kemilembe Joseph, .... Kilichotokea baada ya kulala sikupata fahamu tena. Baadae nimekuja kuzinduka Musa Chibali Semwenda ananinywesha chai na mkate. KUMBE NILIZIMIA KWA NJAA!. Baada ya kupata chakula kile nilipata nguvu kidogo na kisha kwenda zahanati ya chuo na daktari akaniambia ulikuwa umekaa muda mrefu sana bila kula. Mgomo ulipoanza nilishiriki kikamilifu huku nikiwa na maumivu makubwa moyoni kwamba ningekufa kwa njaa mie kama sio kusaidiwa na rafiki mwema. POLICE WANGENIPIGA NA KUNIUA KWA RISASI AMA MABOMU LAKINI NILIKUWA NAJUA NINACHOTETEA.
"SINTOACHA KUPAMBANA KUTETEA WANYONGE WENZANGU HADI PUMZI YANGU YA MWISHO"
Hizi ni salamu kwa Waziri Mkuu Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mtoto wa Mkulima aliyesahau Wakulima wenzie kwa ulevi wa Madaraka) kauli yako ya juzi imezidi kunitia maumivu, na kunikumbusha yale mabomu tuliyopigwa na police miaka 8 iliyopita.

Monday, June 3, 2013

HUTUBA YA MWENYEKITI WA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA

HOTUBA YA MWENYEKITI WA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA, JAJI JOSEPH S. WARIOBA, KATIKA MKUTANO WA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU UZINDUZI WA RASIMU YA KATIBA TAREHE 03 JUNI, 2013 KWENYE VIWANJA VYA UKUMBI WA KARIMJEE,
DAR ES SALAAM.
    Mhe. Dkt Mohammed Gharib Bilali – Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano,
    Mhe. Mizengo K. P. Pinda (Mb.) - Waziri Mkuu,
    Mhe. Seif Sharif Hamad – Makamu wa Kwanza wa Rais – Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
    Mhe. Balozi Seif Ali Iddi (Mb.) - Makamo wa Pili wa Rais - Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
    Mhe. Mathias Chikawe – Waziri wa Katiba na Sheria,
    Mhe. Abubakar Khamis Bakary - Waziri wa Katiba na Sheria wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
    Mhe. Jaji Frederick M Werema - Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
    Mhe. Othman Masoud Othuman - Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar,
    Viongozi wa Vyama vya Siasa,
    Waheshimiwa Wajumbe wa Tume na Wajumbe wa Sekretarieti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
    Ndugu Wananchi,
    Wageni Waalikwa
    Waandishi wa Habari Mabibi na Mabwana.
    UTANGULIZI
Ndugu Wananchi,
Awali ya yote namshukuru mwenyezi mungu kwa kutuwezesha kufikia hatua hii ya leo ya kuzindua Rasimu ya Katiba. pia, niwashukuru ninyi nyote mliohudhuria halfa hii ikiwa ni mwendelezo wa mchakato muhimu wa Mabadiliko ya Katiba ya nchi yetu.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ilipitishwa Bungeni Novemba, 2011 na kufanyiwa mabadiliko Februari, 2012. Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliundwa kwa mujibu wa Kifungu 6(1) cha sheria hiyo (Cap.83). Wajumbe 34 wa Tume waliteuliwa na kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, mwezi Aprili, 2012. Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Tume imepewa miezi kumi na minane kukamilisha kazi yake kuanzia siku ilipoanza kazi rasmi ambayo ilikuwa Mei 2, 2012.
Tume iliandaa ratiba ya utekelezaji wa majukumu yake. Kufuatana na ratiba hiyo Tume ilijipanga kukusanya maoni ya wananchi katika kipindi cha miezi mitano kuanzia Mwezi Julai hadi Disemba, 2012. Kazi hiyo ilifanywa kama tulivyopanga. Tume ilijigawa katika makundi na ilitembelea mkoa yote thelathini.
Tume ilifanya mikutano 1,942 ambayo ilihudhuriwa na wananchi wapatao 1,365,337 ambao kati ya hao wananchi 333,537 walitoa maoni ama kwa mazungumzo ya ana kwa ana au kwa maandishi. Tume pia ilipata maoni ya wananchi wengi, wa ndani na nje ya nchi kwa njia mbali mbali kama vile; Mikutano ya hadhara, Fomu maalum za Tume, barua kupitia Masanduku ya Barua ya Tume, Mitandao ya Kijamii ya barua pepe; facebook ya Tume, Tovuti ya Tume; Makala mbalimbali kutoka kwenye magazeti na ujumbe mfupi wa simu.
Tume ilitumia mwezi Januari, 2013 kukusanya maoni ya makundi mbali mbali katika jamii, ikiwa ni pamoja na vyama vya siasa, taasisi za Serikali, taasisi za dini, wakulima, wafugaji, wafanyakazi, asasi za kiraia na kadhalika. Makundi zaidi ya 160 yalikutana na Tume na kutoa maoni. Tume pia ilipata maoni ya viongozi wa juu wa Serikali walioko madarakani na waliostaafu. Kwa jumla viongozi 43walitoa maoni.
Tume ilipanga kutumia miezi mitatu ya Februari, Machi na Aprili kuchambua maoni ya wananchi na kuandaa Rasimu ya Katiba. Lakini tuligundua kwamba maoni tuliyopata yalikuwa mengi sana, na pamoja na matumizi ya teknolojia ya kisasa, tulitambua umuhimu wa kuongeza muda hadi mwisho wa mwezi Mei, Maoni ya wananchi yaligusa mambo yote yanayohusu Katiba na mengi ya maoni hayo yalikinzana. Aidha, baadhi ya maoni yaligusia masuala ya Kisera, Kisheria na Kiutendaji. Tulifanya uchambuzi makini na wa ndani wa maoni hayo na kazi hiyo tumeikamilisha na rasimu imeandaliwa na Tume na leo tupo hapa kwa ajili ya kuizindua, ambapo Wananchi watapata nafasi ya kuisoma. Kwa leo, kwa niaba ya Tume, napenda kutaja maeneo machache tu ambayo tunayapendekeza.
    IBARA ZINAZOPENDEKEZWA KWENYE RASIMU YA KATIBA
Ndugu Wananchi,
Katiba yetu ya sasa ina ibara 152. Tume ilifanya jitihada kubwa sana kuandaa rasimu ambayo siyo ndefu. Lakini katika hali halisi haikuwezekana. Rasimu ya Katiba tunayopendekeza ina ibara 240.
    MISINGI MIKUU YA TAIFA
Utangulizi wa Katiba ya sasa ndio unaobeba misingi mikuu ya Taifa ambayo ni Uhuru, Haki, Udugu na Amani. Tume inaamini kwamba misingi hii ni mizito na inastahili kubaki kwenye Katiba mpya. Hata hivyo, Tume imeona ni busara kuongeza misingi mingine mitatu ya Usawa, Umoja na Mshikamano. Hivyo, Tume imependekeza Katiba iwe na Misingi Mikuu saba ya Taifa;yaani; Uhuru, Haki, Udugu, Usawa, Umoja, Amani na Mshikamano.
    TUNU ZA TAIFA
Katiba yetu ya sasa haina sehemu inayoelezea tunu za Taifa (National Values). Wananchi wengi walitoa maoni kwamba Katiba itaje Tunu za Taifa. Tume imependekeza Tunu zifuatazo zitajwe ndani ya Katiba. Tunu hizo ni;- Utu, Uzalendo, Uadilifu, Umoja, Uwazi, Uwajibikaji na Lugha yetu ya taifa ya Kiswahili.
    MALENGO YA TAIFA
Tume ilipozunguka nchi nzima wananchi walizungumzia sana kuhusu malengo ya taifa. Walitaka Katiba ionyeshe dira ya taifa. Wananchi wanayo ndoto yao ya Tanzania ya kesho na kesho kutwa. Kwa kuzingatia maoni ya wananchi, kuna sura nzima inayohusu Malengo mahsusi na ya msingi ya mwelekeo wa shughuli za Kiserikali na Sera za Kitaifa. Rasimu ya Katiba inaeleza kuwa Malengo ya Kitaifa yaliyoainishwa ndani ya Rasimu yatakuwa ni Mwongozo kwa Serikali, Bunge, Mahakama, Vyama vya Siasa, Taasisi na Mamlaka nyingine, na kwa kila mwananchi katika matumizi au kutafsiri Masharti ya Katiba au Sheria nyingine za Nchi.
Kwa msingi huo, Tume imependekeza malengo makuu ya taifa yapanuliwe kwa mpangilio wa kuonesha malengo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, kimazingira na sera ya mambo ya nje. Malengo hayo yameingizwa kwenye Rasimu ya Katiba.
    VYOMBO VYA KIKATIBA
Wananchi walizungumzia suala la kubainishwa kwa vyombo vya Kikatiba na kuingizwa kwenye Katiba ili viwe na nguvu ya Kikatiba katika utekelezaji wa majukumu yao. Tume imependekeza baadhi ya vyombo vifuatavyo viwe vya Kikatiba; Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali, Baraza la Mawaziri, Kamati Maalum ya Makatibu Wakuu na Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri; Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa, Tume Huru ya Uchaguzi, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Tume ya Utumishi wa Umma, Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
    MAADILI YA VIONGOZI NA MIIKO YA UONGOZI
Wananchi wengi pia walizungumzia kwa upana sana kuhusu maadili na miiko ya Viongozi, kwa kuzingatia maoni ya wananchi Tume inapendekeza maadili ya viongozi wa umma, pamoja na miiko ya uongozi yawekwe kwenye Katiba. Tume pia imependekeza kuwa Sekretariati ya Maadili ibadilishwe kuwa Tume yenye mamlaka makubwa ya kusimamia maadili ya viongozi wanaovunja miiko ya uongozi.
    HAKI ZA BINADAMU
Kuhusu haki za binadamu wananchi walitaka haki hizi ziimarishwe na kusiwe na vikwazo visivyo vya lazima. Tume imependekeza mabadiliko katika baadhi ya haki za binadamu kwa madhumuni ya kuziimarisha. Moja ya mabadiliko hayo ni kuhusu uhuru wa mwananchi kushiriki shughuli za umma. Tume inapendekeza kwamba vikwazo vilivyowekwa kuzuia mgombea huru viondolewe. Kwa maana nyingine Tume inapendekeza mgombea binafsi aruhusiwe.
Tume pia, inapendekeza haki mpya ziingizwe kwenye Katiba ikiwa ni pamoja na haki ya wafanyakazi, , haki ya mtoto, haki za Watu wenye Ulemavu, Haki za Wanawake, Haki za Wazee, Haki za Makundi Madogo katika Jamii, Haki ya Elimu na Kujifunza, Haki ya kupata habari, Haki na uhuru wa habari na vyombo vya habari na kadhalika.
    URAIA
Wananchi wengi walipendekeza kuwa suala la Uraia libainishwe wazi kwenye Katiba. Tume imependekeza kwa kutaja Raia wa Jamhuri ya Muungano na haki zake.
    MIKOPO NA DENI LA TAIFA
Ndugu Wananchi,
Wananchi walizungumzia suala la uwepo wa Ukomo wa nchi kukopa na uwepo wa utaratibu wa kulipa Deni la Taifa ili kuilinda Nchi isiwe na deni kubwa. Kwa kuzingatia maoni ya Wananchi, Tume imependekeza kuwa, Serikali itawajibika kutoa taarifa Bungeni kuhusu Mikopo kwa kuainisha kiasi cha deni lililopo, riba yake na matumizi ya fedha za Mikopo na utaratibu wa kulipa Madeni ya Taifa.
    MFUMO WA UTAWALA
Kuhusu utawala, Tume inapendekeza Tanzania iendelee na mfumo wa Jamhuri kwa maana ya nchi inayoongozwa na Rais Mtendaji ambaye ni Mkuu wa nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu.
  UCHAGUZI WA RAIS
        Umri wa kugombea Urais
Tume ilipokea maoni yanayokinzana kuhusu umri wa mwananchi kugombea Urais. Baadhi walipendekeza mtu akishakuwa na sifa ya kupiga kura awe pia na sifa ya kugombea Urais. Umri wa mtu kuruhusiwa kupiga kura ni miaka 18. Wengine walipendekeza umri uliopo kwenye Katiba wa mtu kugombea Urais, yaani kuanzia miaka 40 na kuendelea, uendelee kubaki kama ulivyo.
Wengine walisema Umri wa mtu kuruhusiwa kugombea Urais uwe miaka 35 au miaka 50 na kuendelea.
Tume imeyachambua maoni yote hayo, ikafanya utafiti kwa kupitia Katiba za Nchi zingine na uhalisia wa watu wanaogombea na kuchaguliwa kuwa Marais katika Nchi mbalimbali Duniani ambazo zingine zimeruhusu wagombea wa nafasi ya Urais kuwa na umri chini ya miaka 40.
Wengi walioomba kugombea nafasi hiyo walikuwa na umri wa miaka 40 au zaidi.
Kwa kuzingatia maoni ya wananchi, utafiti na hali halisi, Tume inapendekeza Rais aendelea kuchaguliwa na wananchi na pamoja na sifa nyingine, mtu anayeomba urais asiwe chini ya miaka 40.
Uchaguzi wa Rais itakuwa kama ilivyo sasa, yaani mgombea Urais atakuwa na mgombea mwenza kwa utaratibu kama ilivyo sasa. Isipokuwa, Tume imependekeza Mgombea Urais anaweza kupendekezwa na Chama cha Siasa au kuwa Mgombea Huru.
Mgombea wa nafasi ya Rais atatangazwa kuwa mshindi iwapo atakuwa amepata kura zaidi ya asilimia hamsini ya kura zote zilizopigwa.
Hata hivyo, matokeo ya uchaguzi wa Rais yanaweza kulalamikiwa Mahakamani, lakini siyo kila mtu anaweza kufungua kesi. Wanaoweza kufungua kesi ni wagombea Urais. Aidha, ni Mahakama ya Juu pekee ndiyo itakuwa na Mamlaka na uwezo wa kusikiliza malalamiko kuhusu matokeo ya uchaguzi wa Rais na shauri lazima liamuliwe ndani ya mwezi mmoja, yaani siku therathini.
Rais aliyeshinda ataapishwa siku thelathini tangu alipotangazwa kuwa mshindi au kuthibitishwa na Mahakama.
    MADARAKA YA RAIS
Ndugu Wananchi,
Tume inapendekeza kwamba, Rais abaki na madaraka ya uteuzi wa viongozi wa ngazi za juu. Hata hivyo inapendekezwa Rais ashirikiane na taasisi na vyombo vingine katika uteuzi. Kwa mfano:
Uteuzi wa Mawaziri na Manaibu Waziri, Rais atateua na Bunge litathibitisha.
Kuhusu Jaji Mkuu na Naibu Jaji Mkuu Rais atawateua kutokana na majina ya watu waliopendekezwa na Tume ya Uutumishi wa Mahakama na baada ya hapo Bunge litathibitisha.
Kuhusu Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama inapendekezwa kianzishwe chombo kipya kitakachoitwa Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa, ambalo kati ya majukumu yake itakuwa ni kumshauri Rais kuhusu uteuzi wa Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Kuhusu Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu watateuliwa na Rais kutokana na mapendekezo ya Tume ya Utumishi wa Umma.
    KINGA YA RAIS
Tume baada ya kupitia maoni ya Wananchi, inapendekeza Rais abaki na kinga kama ilivyo sasa na anaweza kushitakiwa na Bunge kama ilivyo Katiba ya sasa.
IDADI YA MAWAZIRI
Inapendekezwa Rais aunde Serikali ndogo iliyo na Mawaziri wasiozidi kumi na tano na mawaziri hao wasiwe wabunge. Mawaziri hawatahudhuria vikao vya Bunge isipokuwa kama watahitajika kutoa ufafanuzi kwenye kamati za Bunge.
    BUNGE
Ndugu Wananchi,
Kuhusu Bunge kutakuwa na wabunge wa aina mbili. Kutakuwa na Wabunge wa kuchaguliwa na wabunge watano wa kuteuliwa na Rais kuwakilisha Watu wenye Ulemavu
Kila Jimbo la Uchaguzi litakuwa na Wabunge Wawili mmoja mwanamke na mwingine mwanamume.
Tume inapendekeza kwamba, Mbunge akifukuzwa na Chama cha Siasa abaki kuwa Mbunge lakini akihama Chama atapoteza Ubunge wake.
Inapendekezwa ukomo wa Ubunge uwe vipindi vitatu vya miaka mitano mitano. Hata hivyo, wananchi wanaweza kumwondoa mbunge wao kabla ya mwisho wa kipindi chake.
Inapendekezwa pia kusiwepo na uchaguzi mdogo isipokuwa kama nafasi inayokuwa wazi inatokana na Mbunge huru ndipo utafanyika uchaguzi mdogo kujaza nafasi hiyo, lakini kama nafasi ikiwa wazi kutokana na Mbunge wa Chama cha Siasa basi nafasi hiyo, ijazwe na mtu kutoka Chama hicho.
Inapendekezwa Spika na Naibu Spika wasitokane na Wabunge na wasiwe Viongozi wa vyama vya Siasa.
    TUME YA UCHAGUZI
Tume imefanya uchambuzi wa maoni ya wananchi kuhusu Tume ya Uchaguzi. Tume inapendekeza jina la tume liwe Tume Huru ya Uchaguzi. Tume pia inapendekeza sifa za wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi ziwekwe kwenye Katiba. Wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi watapatikana kutoka miongoni mwa watu wenye sifa zilizoainishwa ndani ya Katiba kwa kuomba. Majina ya waombaji yatachambuliwa na Kamati ya Uteuzi ambayo Mwenyekiti wake atakuwa Jaji Mkuu na wajumbe wengine sita ambao ni Majaji Wakuu wa nchi Washirika, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Maspika wa Mabunge wa nchi Washirika na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu.
Kamati ya uteuzi itapendekeza majina ya watu wanaofaa kwa Rais ambaye atateua Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wengine. Bunge litathibitisha uteuzi wao. Wabunge na viongozi wa aina hiyo hawatakuwa na sifa za kuwa wajumbe wa tume ya uchaguzi.
Inapendekezwa Tume huru ya Uchaguzi isimamie masuala ya uchaguzi, kura ya maoni na Usajili wa Vyama vya Siasa.
    MAHAKAMA
Kuhusu Mahakama inapendekezwa kuanzishwa kwa Mahakama ya Juu (Supreme Court) Majaji wa Mahakama ya Juu na Mahakama ya Rufani watateuliwa na Rais baada ya kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.
    MUUNDO WA MUUNGANO
Ndugu Wananchi,
Suala la muundo wa Muungano ndilo lililokuwa gumu kuliko masuala yote. Tume ilitumia muda mwingi kuchambua maoni ya wananchi. Pamoja na kwamba hadidu za rejea zilielekeza Tume kuzingatia uwepo wa Muungano, baadhi ya wananchi walitoa maoni kwamba Muungano uvunjwe na Tume iliyapokea maoni hayo. Licha ya kwamba waliotaka kuvunjwa muungano walikuwa wachache sana, Tume ilichambua sababu walizotoa na kuridhika kwamba hazikuwa na uzito.
Wananchi walio wengi walitaka Muungano uendelee. Kati yao wapo waliopendekeza Muungano wa Serikali moja, Serikali mbili, Serikali tatu, Serikali nne na muungano wa mkataba. Sababu za wale waliopendekeza Serikali nne hazikuwa na uzito, kwa hiyo Tume ikaamua kutopendekeza muundo huo.
Wananchi waliopendekeza Serikali moja walikuwa wachache lakini sababu zao zilkuwa na uzito. Hata hivyo, Tume kwa kuzingatia hali halisi iliona ni changamoto kubwa kuwa na Muungano wa Serikali Moja.
Wananchi waliopendekeza Muungano wa Mkataba walikuwa wengi (hasa wananchi wa Zanzibar) na sababu zao zilikuwa na uzito. Lakini uchambuzi wa Tume ilionekana wazi kwamba ili kupata mkataba lazima kwanza kuwe na nchi mbili huru kabisa lakini hakukuwa na mazingira ya uhakika ya kupata mkataba wa muungano. Tume iliona kuna changamoto ya muungano kuvunjika ingawa waliotoa maoni walisisitiza muungano ubaki. Hivyo, Tume iliamua kutopendekeza muundo huo.
Wananchi waliopendekeza Tanzania iendelee na Muundo wa sasa wa Serikali mbili walikuwa wengi na sababu zao zilikuwa nzito. Hata hivyo, wananchi katika kundi hili walipendekeza mabadiliko mengi na makubwa. Tathmini ya Tume ilionyesha kwamba isingewezekana kufanya mabadiliko yote yaliyopendekezwa.
Wananchi waliopendekeza muundo wa Serikali tatu walikuwa wengi kuliko makundi yote. Sababu zao zilikuwa nzito lakini pia kulikuwa na changamoto nyingi na nzito. Pamoja na maoni ya wananchi Tume ilirejea sababu za kupendekeza muundo huu zilizotolewa na Tume zilizopita na Tafiti zilizofanywa na Tume kuhusu aina mbalimbali za Muungano. Baada ya yote hayo Tume ilifikia uamuzi wa kupendekeza mfumo wa Serikali tatu. Yaani Serikali ya Shirikisho, Serikali ya Tanzania Bara na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
    ORODHA YA MAMBO YA MUUNGANO
Ndugu Wananchi,
Tume imependekeza katika Rasimu ya Katiba kuwa orodha ya Mambo ya Muungano yawe 7 badala ya 22 yaliyopo sasa.
Mambo ya muungano yanayopendekwa ni:
    Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
    Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
    Uraia na Uhamiaji
    Sarafu na Benki Kuu
    Mambo ya Nje
    Usajili wa Vyama vya Siasa
    Ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya Kodi yatokanayo na Mambo ya Muungano.
    BENKI KUU
Kwa kuwa Tume imependekeza Muungano wa Shirikisho kutokana na uzito wa maoni ya wananchi. Hivyokutakuwa na Benki Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakayokuwa na wajibu wa kusimamia masuala ya Sarafu na Fedha za Kigeni na Benki za Washirika wa Muungano.
    BENKI ZA SERIKALI ZA WASHIRIKA
Kutokana na pendekezo la kuwepo kwa Serikali ya Shirikisho la Nchi tatu, inapendekezwa kuwepo kwa Benki zitakazokuwa na jukumu la kutunza akaunti ya fedha za Serikali za kila Mshirika wa Muungano na kuzisimamia benki za biashara katika mamlaka zao.
    BAADHI YA MAMBO AMBAYO HAYAMO KWENYE RASIMU YA KATIBA
        Serikali ya Majimbo
Ndugu Wananchi,
Tume ilipokea maoni kuhusu mambo mengine muhimu ambayo hayamo katika rasimu hii. Moja ya mambo hayo ni Serikali za Majimbo. Tume ilichambua maoni na sababu za wananchi kupendekeza Serikali za Majimbo lakini Tume ilibaini changamoto nyingi na ikaamua kutopendekeza muundo huu.
Kwanza, baada ya kuamua kupendekeza Muundo wa Muungano wa Serikali Tatu, ilionekana ni dhahiri kuongeza ngazi nyingine ya Serikali ingeleta gharama kubwa. Serikali nyingine kumi zingekuwa na Wakuu wa Majimbo, Mabaraza ya Mawaziri na Mabunge na gharama yake ingekuwa kubwa.
Pili, katika kutembelea nchi Tume ilishuhudia dalili za wazi za mivutano ya Udini, ukanda,malalamiko ya upendeleo wa baadhi ya maeneo na ukabila. Dalili zilikuwa wazi kwamba utawala wa majimbo ungeirudisha nchi kwenye utawala utakaoigawa nchi kwa misingi ya ukabila, udini na ukanda na kuzigawa rasilimali za taifa kikanda na hivyo kuleta tofauti kubwa ya kimaendeleo katika nchi.
    Mahakama ya Kadhi
Ndugu wananchi,
Jambo la pili ni mahakama ya kadhi. Tume ilipokea maoni mengi kuhusu suala hili. Baadhi ya wananchi walitaka mahakama ya kadhi iingizwe kwenye Katiba na wengine walipinga. Baada ya kuamua kuwa Muundo wa Muungano uwe wa Serikali Tatu, Tume iliona kuwa Mahakama ya Kadhi siyo suala la Muungano na imeliacha ili lishughulikiwe na Washirika wa Muungano.
Hata hivyo ilionekana kuwa suala siyo kuwapo au kutokuwapo kwa mahakama ya kadhi. Mahakama hizo zinaweza kuwapo bila ya kuwa katika Katiba. Zanzibar kuna mahakama ya kadhi bila kuingizwa kwenye Katiba ya Zanzibar. Kwa kutumia uzoefu huo hata Tanzania Bara inaweza kupata ufumbuzi wa suala hili.
    Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya
Jambo la Tatu ni Kuwepo au kutokuwepo kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya. Baadhi ya Wananchi walitaka Wakuu wa Mikoa na Wilaya wasiwepo, wengine walitaka Wakuu wa Mikoa na Wilaya waendelee kuwepo lakini wachaguliwe na wananchi na waengine wakasema wawepo na waendelee kuteuliwa na Rais kama ilivyo sasa. Tume ilitafakari kuhusu suala hili na kuamua kwamba siyo suala la Muungano na kwa kuwa Muundo wa Muungano imependekezwa uwe wa Serikali Tatu, Tume iliona suala la uwepo au kutokuwepo na namna ya upatikanaji wa Wakuu wa Mikoa na Wilaya lishughulikiwe na Washirika wa Muungano.
    Serikali za Mitaa
Kuhusu Serikali za Mitaa, Tume ilipokea maoni kutoka kwa wananchi kuhusu kuziimarisha Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuzipatia uhuru kamili wa kujiamulia mambo yao bila kuingiliwa na Serikali Kuu. Tume ilitafakari suala hili na kuamua kwamba siyo jambo la Muungano na hivyo, litashughulikiwa kwenye Katiba za Washirika wa Muungano.
    Uraia wa Nchi mbili
Ndugu Wananchi,
Jambo la tatu ni Uraia wa Nchi mbili. Tume ilipokea maoni kutoka kwa wananchi mbalimbali kuhusu kuwekwa kwenye Katiba suala la Uraia wa nchi mbili. Baada ya kufanya uchambuzi kwa kutengenisha mambo yapi ni ya Kikatiba na yapi yanaweza kutekelezwa bila kuingizwa kwenye Katiba bali kwenye Sheria inayohusu jambo husika, Tume imependekeza kuwa suala la Uraia wa nchi mbili linaweza kuwekwa kwenye Sheria badala ya kuwekwa kwenye Katiba. hii ni kwa sababu kutokana na utafiti uliofanywa na Tume, suala hilo linaweza kubadilika wakati wowote na hivyo likiwa kwenye Katiba linaweza kuifanya Katiba kubadilishwa mara kwa mara.
MWISHO
Naomba nichukue fursa hii kwa niaba ya Tume kuwashukuru Watanzania wote kwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Mabadiliko ya Katiba, kuanzia hatua ya kutoa maoni na kuwachagua wawakilishi wenu watakaopata fursa ya kuipitia, kuijadili na kuitolea maoni Rasimu ya Katiba. Ushirikiano huu ulikuwa muhimu sana kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba hasa ukizingatia kuwa lengo ni kupata Katiba Mpya ambayo itaakisi ndoto na matakwa ya Wananchi wa Tanzania.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, inatoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar:
    Kwa kuipatia vifaa afisi na mahitaji ya lazima
    Kwa kuiwezesha Tume kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu,
    Kwa kutokuingilia Uhuru wa Tume wakati wa Utekelezaji wa Majukumu yake na
    Kutoa Wataalam wenye Weledi, Mahiri, Makini na Waadilifu ambao wameunda Sekretarieti ya Tume.
Ndugu Wananchi,
Shukrani za pekee ziwaendee:
    Wakuu wa Mikoa,
    Wakuu wa Wilaya,
    Wakurugenzi / Makatibu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa,
    Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Wilaya,
    Watendaji wa Kata, Vijiji, Mitaa na Masheha.
Kwa kuisaidia Tume kutekeleza Majukumu yake kwa ufanisi. Aidha, tunazishukuru Asasi za Kiraia, Taasisi, Jumuiya za Kidini, Vyama vya Siasa na Makundi mbalimbali kwa namna walivyoshiriki katika kuhamasisha wananchi kushiriki katika kutoa maoni.
Mwisho ingawa siyo kwa umuhimu, Tunawashukuru Wanahabari wote kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuisaidia Tume kufikisha taarifa mbalimbali za Tume kwa Wananchi na katika kuhamasisha Wananchi kushiriki katika mchakato wa Mabadiliko ya Katiba.
Nachukua nafasi hii kuwaomba Wananchi kupitia Mabaraza ya Katiba ya Wilaya, Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi ya Watu wenye Malengo yanyofanana kushiriki vyema, kwa umakini, utulivu na kwa amani katika hatua hii ya kuipitia, kuijadili na kuitolea maoni Rasimu ya Katiba.
Tume imekuwa ikithamini na itandelea kuthamini mawazo na maoni kutoka kwa Watanzania wote.
Rasimu ya Katiba itapatikana kwenye tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya www.katiba.go.tz
SASA NAKUOMBA MHESHIMIWA MAKAMU WA RAIS UIZINDUE RASMI RASIMU YA KATIBA
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
TOA MAONI TUPATE KATIBA MPYA

Thursday, May 30, 2013

WENJE AZUA BALAA LINGINE BUNGENI!

SEHEMU YA HUTUBA YA KAMBI YA UPINZANI ILIYOZUA BALAA!
3.0. VYAMA VYA SIASA NA MISAADA KUTOKA NJE YA NCHI.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa ‘United Nations University’(UNU-WIDER) ya mwezi Aprili 2012 iliyoandaliwa na Aili Mari Tripp ilionyesha kuwa misaada ya wahisani kutoka nje katika mabadiliko ya kisiasa Tanzania ‘Donor Assistance and Political Reform in Tanzania’, inaonyesha kuwa Tanzania imepokea misaada kutoka nje yenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 26.85 toka mwaka 1990-2010.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti hiyo ni kuwa Tanzania ni nchi inayoongoza kusini mwa jangwa la Sahara kwa kupokea misaada mingi kutoka nje ya nchi na hasa kutoka mataifa ya Ulaya na taasisi za nchi za Uingereza, Marekani, Ujerumani, Uholanzi, Norway, Canada, Sweden, na taasisi kama Benki ya Dunia, IMF ,UNDP ,UNICEF na mengineyo.
Pamoja na misaada yote hiyo, bado tumeendelea kuwa nchi maskini sana duniani pamoja na kuwa na rasilimali lukuki ambazo tumepewa na Mungu ila tunashindwa kuzitumia kwa manufaa ya watanzania na badala yake tumeendelea kudanganywa na vimisaada vidogo vidogo na kubadilishana na rasilimali zetu kama madini, misitu ,wanyama nk kwa ajili ya misaada hiyo.
Mheshimiwa Spika, pamoja na misaada hiyo kwa serikali hii ya CCM bado vyama vya siasa vimekuwa na mahusiano na baadhi ya vyama vingine vya siasa katika mataifa ya magharibi na vimekuwa vikipokea misaada ya aina mbalimbali kama fedha , nyenzo na mengineyo kadiri ya makubaliano na mirengo ya kiitikadi ya vyama husika.Pamoja na ukweli huo bado vipo vyama vya siasa vinavyopotosha umma kuhusiana na misaada vinayopokea kutoka nje ya nchi na vyama hivi vimekuwa mstari wa mbele kueneza propaganda za uongo kuwa vyenyewe havipokei misaada kutoka nchi za magharibi.
Mheshimiwa Spika, CCM wao ‘wanajiita’ kuwa wapo mrengo wa kijamaa/kikomunisti na wamekuwa wakipokea misaada mingi sana ya fedha na nyenzo kutoka Umoja wa Vyama vya Kikomunisti Ulimwenguni ‘Socialist International’ kutoka katika nchi kama za Ujerumani kupitia SDP ,Uingereza kupitia chama cha Labour,China kupitia chama cha Kikomunist ,Marekani kupitia chama cha Democrats. Pamoja na misaada ya kifedha na kiufundi ambayo CCM imekuwa ikipata kutoka nje wamekuwa hawatangazi hadharani hata mara moja kuhusiana na kiasi ambacho wamekuwa wakipokea na hivyo kila kitu kwao imekuwa ni siri kuu ya viongozi wao.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa chama cha CUF, kutokana na itikadi zake za mrengo wa Kiliberali ambazo miongoni mwa misingi yake mikuu ni pamoja na “kupigania haki za ndoa ya jinsia moja, usagaji na ushoga”. Hii ni kwa mujibu wa tangazo lao kwenye mtandao wao wa umoja wa maliberali ulimwenguni, likiungwa mkono na Waziri wa Haki na Usawa wa Uingereza, Lynn Featherstone kutoka chama cha Liberal Democrats wakati chama hicho(www.liberal-international.org) kilipokuwa kinapitisha azimio la kuruhusu ndoa za jinsia moja kama haki ya mtu mmoja mmoja, wanashirikiana na vyama kama vile LPC ya Canada, Det Radikale Venstre cha Norway, FDP cha Ujerumani, Israel Liberal Group cha Israel,PDS cha Senegal na Liberal Democrats cha Uingereza.
Kutokana na umoja huo, CUF wamekuwa wakipata msaada wa kifedha na nyenzo nyingine mbalimbali kutoka kwa vyama hivyo vya mrengo wa Kiliberali na msaada wa mwisho ni hivi majuzi mwezi Machi 2013 waliposaini makubaliano na chama cha Kiliberali kutoka Norway.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa CHADEMA, wapo kwenye Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Ulimwenguni (International Democratic Union - IDU). Huu ni umoja wa vyama ambavyo vipo kwenye mrengo wa kati na ambavyo msingi wake mkuu ni pamoja na kuwa na familia, kama taasisi muhimu katika jamii, ikimaanisha kwamba: “tunapinga vitendo vyote vya ushoga na usagaji”. Tunatetea demokrasia, haki za binadamu na kupambana na ufisadi katika serikali. Vyama wanachama wa umoja huu ni pamoja na Conservative Party cha UK, CPP cha Norway, Republican cha Marekani na vingine vinavyofuata mrengo huo.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya upinzani Bungeni, inavitaka vyama vyote ambavyo vimekuwa na mahusiano na vyama vya nje viweke wazi mikataba yao na malengo ya mahusiano hayo ikiwa ni pamoja na misaada ambayo vimekuwa vikipokea kutoka kwenye nchi hizo .
MTIRIRIKO WA MATUKIO KUTOKA KWA MOJA YA WADAU WALIOKUWA WAKIFUATILIA HOTUBA HIYO!
Ninaandika kwa haraka sijui kama nitakuwa sahihi.
Ni kwamba Waziri Membe katoa hotuba yake ya wizara ya nje. Kisha kafuata Juma Nkamia makamu mwenyekiti wa Kamati husika naye katoa maoni yake.
Kisha ikaja zamu ya Hotuba ya kambi ya upinzani iliyosomwa na Mh. Wenje. Wakati anasoma halikuonekana jambo baya hadi alipofikia. Lakini mnajua kwamba wenzetu mle bungeni hupewa hotuba nzima na wapo walifikia hadi mwisho.
Ndipo mbunge mmoja wa CUF akasimama kwa kutumia kanuni ya ORDER, na kusema tatizo lililomo kwenye hotuba ile.
Mbunge yule akasoma nadhani ni ukurasa wa nane akisema kwamba hotuba inataja chama cha CUF kama chama chenye mlengo wa Liberal ambapo duniani inajulikana mlengo huo unashabikia ndoa za ushoga.
Hivyo, mbunge akaamuru hotuba hiyo, si tu isisomwe, bali CHadema waombe radhi kwa sababu CUF si chama cha mashoga. Na isipofanyika hivyo, basi CUF watafungua kesi kuishitaki Chadema na kulishitaki bunge.
Wakati anasema vipaza sauti vingi tu vikashangilia kwamba yeye mwenyewe huyo Wenje ndiye anayestahili matusi hayo.
Naibu Spika alipomaliza kumsikiliza mbunge huyo wa CUF, akainuka na kumpa nafasi Wenje ajieleze kama ana neno lolote kuhusu taarifa hiyo.
Wenje akainuka na kuanza kufafanua. Akafafanua kwamba kuhusu mlengo hawakuitaja CUF tu, wameitaja CCM kwamba ni chama kina mloengo wa leftist. Wao kama Chadema wamejitaja wako mlengo wa kati. Lakni CUF wametajwa kuwa wako mlengo wa liberal.
Hivyo, milengo hiyo iko katika basis ya ideology. na ma-liberal wanajulikana duniani ndiyo watetezi wakubwa wa ushoga.
Kabla hajamalizia kusema mh. Wenje, wabunge karibu wengi nadhani ni wa CUF wakainuka na vipaza sauti vikawa vinasema kila mmoja na lwake.
Ikawa vurugu ingawa sikuona Naibu Spika akitoa mtu nje au kuita askari wa bunge. Hivyo, akaamua kusitisha vikao vya bunge na akaita nadhani kamati mojawapo ikutane kujadili hotuba hiyo.
Hayo ndiyo yaliyojiri dakika tano zilizopita.
Samahani kama flow ya details haikuwa nzuri


RIPOTI YA DAKTARI JUU YA KILICHOSABABISHA KIFO CHA MSANII WA BONGO FLAVA ABERT MANGWEA!


  Kwa mujibu wa ripoti hiyo kutoka hospitali alikopelekwa marehemu Ngwair, Dkt. Shirley Radcliffe amethibitisha kuwa kilichomuua Albert Mangwair ni sumu ya kilevi. [Ufafanuzi wangu] Kilevi au alkoholi inayolewesha watu kwenye pombe ni sumu. Ukiinywa kwa kiwango kikubwa, kinaweza kukusababishia upotevu wa fahamu, kupunguza uwezo wa kupumua, na hata kifo.
Taarifa hiyo inaendelea kwa kusema kwamba baada ya kunywa kupita kiasi, Ngwair alitumia mihadarati kwa kiwango kikubwa kuliko mwili wake unavyoweza kuhimili(drug overdose)iliyoko kwenye pombe. Dkt Radcliffe aliongeza kuwa Ngwair alipelekwa katika wodi ya watu mahututi kutokana na upungufu mkubwa wa oksijeni mwilini au “hypoxemia.”
Mmoja wa rafiki zake alikuta chupa mbili za vodka zikiwa tupu ndani ya gari, na Ngwair alikua na tatizo la kula linaloitwa bulimia kwa miezi kadhaa kabla ya kifo chake, ambapo alikua akijirusha bila kikomo bila kupumzika au kupumzika kidogo.
Sampuli ya kutoka tumboni kwake inaonyesha mchanganyiko wa kiwango kikubwa cha mihadarati aina ya cocaine, na heroine, na pia alikutwa akiwa na gramu 0.08 za bhangi kwenye damu.
Kifo chake kilisababishwa na massive heart attack (shambulizi la moyo?) na kushindwa kupumua, vilivyosababisha moyo wake usimame na akafariki baada ya sekunde kadhaa

Wednesday, May 15, 2013

ZITTO KABWE APIGA MARUFUKU WABUNGE WA CHADEMA KUISIFIA SERIKALI YA CCM!

Tumekuwa na uungwana wa kitambua juhudi mbali mbali za serikali katika kuleta maendeleo nchini. Mara kadhaa Mimi binafsi, Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Wabunge wa CHADEMA tumekuwa tukitambua juhudi hizo. Hata hivyo "appreciation" yetu ya nia njema Kabisa imekuwa ikichukuliwa kisiasa na Mawaziri wa CCM na hivyo kutubeza. Leo Waziri Magufuli kaja na flash disk yenye kauli ya ndugu Mbowe huko Hai. Pia kabeza wabunge wengi wa upinzani. Nikiwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni, nimeagiza kwamba kuanzia Leo Ni marufuku Kwa mbunge wa CHADEMA ku appreciate kazi ya Serikali. Uungwana wetu usitumike kutuponza. Tufanye kazi yetu ya kuisimamia Serikali

Tuesday, May 14, 2013

VITIMOTO WATINGA BUNGENI NAIROBI KENYA!

Waandamanaji waamepeleka Kitimoto Bungeni Nairobi Kenya, wamefanya hivyo kwa madai kuwa Wabunge wanajiongezea mishahara ni Walafi kama Kitimoto Wakati Wafanyakazi wa Kawaida hawaongezewi mishahara na maisha ni magumu kwa wote.

WADAU WA TWITTER MPO?, MENGI KUTOA MILIONI MOJA KILA MWEZI

Upo kwenye Twitter? Kama haupo fanya haraka ujiunge sababu kuna ulaji huko!! Mwenyekiti mtendaji wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi amesema kuanzia mwezi huu, atakuwa akitoa shilingi milioni 1 kwa kila tweet itakayomfurasha.
Mengi anataka umkune mtima wake kwa tweet yenye akili ambayo inaweza kuchangia kwa namna moja ama nyingine kupunguza umaskini uliokithiri nchini.
“Umaskini umekuwa sugu. Kwa mwaka1 kuanzia Mei nitatoa sh1m kila mwezi kwa tweet nitakayochagua kuwa bora kushinda vita dhidi ya umaskini,” ametweet leo.
Ameongeza kuwa Tweet hiyo iende kwake, yaani mtu akiandika tweet afanye kummention ili aione. Hiyo ndiyo habari ya mjini....kazi  kwenu wazee wa Twiraaaaa..........

Sunday, May 12, 2013

MWIGULU NCHEMBA NA USHAHIDI ULIOOTA MBAWA DHIDI YA UGAIDI WA LWAKATARE!

UAMUZI wa Mahakama Kuu ya Tanzania kumfutia mashtaka ya ugaidi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare, umekiweka katika mazingira magumu Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa.



Mazingira hayo magumu yanatokana na kuwepo kwa taarifa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba, ambaye baadhi ya wachambuzi wanasema ndiye mwasisi wa dhana ya ugaidi wa Lwakatare, alipanga kutumia kesi hii kama turufu ya kuiumiza CHADEMA inayoonekana kuwa tishio kwa chama tawala.



Vyanzo vyetu vya taarifa vinasema CCM ilitumia rasilimali nyingi kuchonga suala hili, ikitarajia kulitumia kuidhoofisha CHADEMA inayoonekana kuimarika hatua kwa hatua na kutishia mustakabali wao kuelekea uchaguzi mkuu ujao.



CHADEMA sasa ndicho chama kinachoinyima usingizi CCM kiasi cha makada wake kupanga mbinu mbalimbali za kukiua ikiwemo kudai ni chama cha kikabila, kidini na kigaidi; mbinu ambazo huko nyuma walizitumia dhidi ya Chama cha Wananchi (CUF) kilichokuwa tishio.



Licha ya mbinu mbalimbali za kuiua CHADEMA, hali ya mambo bado inaonekana kuwa ngumu zaidi kwa CCM, kwani wananchi wanaonekana kuzipuuza, na hujuma hizi zimekuwa zikivuja kabla ya kutekelezwa.



Wachambuzi wa masuala ya siasa wamelidokeza Tanzania Daima Jumapili kuwa kukwama kwa mbinu hizo za CCM ni dalili za wananchi kuchoshwa na utawala wa chama hicho na kuimarika kwa CHADEMA, ambayo imejipambanua kuwatafutia wananchi ukombozi wa pili.



Baadhi ya wanachama wa CCM wanaojipambanua kama makada makini, wamesema mbinu za kigaidi anazotumia Mwigulu na wenzake wakidhani wanaidhuru CHADEMA, zinaweza kukimaliza chama chao kwa kuwa wananchi wa sasa wana uelewa mpana kuliko miaka kadhaa iliyopita.




Majigambo ya Mwigulu


Katika hali ya kushangilia hujuma walizokuwa wamepandikiza dhidi ya CHADEMA, huku chama hicho kikisisitiza kuwa tuhuma za ugaidi zilikuwa za kupika, Mwigulu alijigamba bungeni Aprili 12 mwaka huu, kuwa ana ushahidi mzito wa ugaidi wa Lwakatare, na kwamba alikuwa tayari kuutoa popote, duniani au mbinguni.



Mwigulu amekuwa akihusishwa na mikakati ya kuimaliza CHADEMA, na inasemekana anaungwa mkono na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, ambaye amewahi kumsifia kwa jinsi “anavyoichachafya CHADEMA”. Wadadisi wa kisiasa wanasema sifa alizopewa na Rais Kikwete zilichangia kumpatia cheo cha unaibu Katibu Mkuu wa CCM, ambacho anakitumia zaidi kufanya propaganda dhidi ya CHADEMA kuliko kujenga chama chake.



Hata hivyo, tambo zake zimeota mbawa baada ya mahakama kumfutia Lwakatare mashtaka ya ugaidi.



Mei 8, mwaka huu, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam ilimfutia mashtaka ya ugaidi Lwakatare kwa hoja kuwa hapakuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha kwamba alikusudia kutenda jinai ya ugaidi kama ilivyodaiwa na jamhuri.



CHADEMA imekuwa ikisema kuwa tuhuma hizo za ugaidi ni za kupanga kwa malengo ya kisiasa, na kwamba Mwigulu ndiye amekuwa akishirikiana na baadhi ya maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa kutengeneza video ya uongo dhidi ya Lwakatare na chama chake.



Hoja ya vyombo vya dola kubambikizia kesi wananchi imeungwa mkono na Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Issa Ponda, ambaye mara baada ya kupewa adhabu ya kifungo cha nje cha mwaka mmoja, alisema ni tabia iliyoota mizizi ya polisi kuwabambikiza kesi wananchi wasio na hatia.



Wakati hoja ya kuwabambikia kesi watu ingali ikiendelea, juzi Jeshi la Polisi mkoani Morogoro limewatia mbaroni askari wake watatu kwa tuhuma za kumbambikia fuvu la kichwa cha mtu mfanyabiashara mmoja wakimshinikiza awape sh milioni 25 ili wamuachie.



Wakati CCM ikionekana kuhaha kutafuta mbinu za kukabiliana na CHADEMA baada ya kushindikana kwa ugaidi, Katibu Mkuu wa chama hicho kikuu cha upinzani, Dk. Willibrod Slaa aliweka wazi kuwa chama tawala kisitarajie mbinu ilizotumia miaka ya nyuma kuudhoofisha upinzani zitafanya kazi sasa.



Dk. Slaa katika mahojiano yake na Tanzania Daima, katikati ya wiki alisema CHADEMA haitolipa kisasi kwa makada wa CCM wanaofanya mbinu chafu za kuudhoofisha upinzani.



“CCM ilizoea kununua wananchi; zamu hii itakuwa na wakati mgumu, ilizoea kuiibia CHADEMA, sasa mambo ni magumu ijiandae kwa pigo kuu,” alisema.



Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wamesema kuwa hatua ya mahakama kufuta mashtaka ya ugaidi dhidi ya Lwakatare yameinusuru zaidi CCM kuliko CHADEMA, kwani kama kesi ingeendelea chama hicho cha upinzani kilikuwa kimeandaa ushahidi mkali ambao ungeiumbua CCM, serikali na Jeshi la Polisi.




Waziri afunguka


Tanzania Daima Jumapili, lilimtafuta Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe azungumzie kufutwa kwa kesi ya ugaidi na watu kubambikiziwa kesi, ambapo alisema vyombo vya dola vinatekeleza majukumu yake kulingana na taratibu walizojiwekea.



Alisema serikali haina tatizo na hukumu ya Mahakama Kuu, kwani imetekeleza kazi zake kwa mujibu wa sheria na yeyote anayehusisha na masuala ya siasa huu ni mtazamo wake.



“Mimi ndiye msimamizi wa mahakama, kwahiyo nakubaliana na hukumu ya Lwakatare, najua mahakama imetekeleza wajibu wake na kazi zake kwa mujibu wa sheria, sina tatizo na hukumu hiyo,” alisema Chikawe.


Wanasheria wanena


Akitoa maoni ya mtazamo wa kisheria kuhusu uamuzi wa Mahakama Kuu, wakili na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Helen Kijo-Bisimba alisema sura ya awali kabisa kuhusu mashtaka ya serikali dhidi ya Lwakatare haikuonesha ushahidi wa kutosha au mazingira ya kutendeka kwa kosa la ugaidi.



“Sijaisoma ile hukumu ya Mahakama Kuu ili kujua kwanini jaji alifikia uamuzi huo, lakini ninachoweza kusema kwa uhakika kabisa ni kwamba hapakuwa na ushahidi wowote wa maana wa kuthibitisha kosa la ugaidi, hapakuwa na kosa la ugaidi pale, na nadhani mahakama imezingatia ukweli huo,” alisema Bisimba.



Mmoja wa mawakili wa Lwakatare, Peter Kibatara alisema kuwa kwa sasa wanaandaa mipango ya kumtoa mahabusu kwa dhamana mteja wao, kwani shtaka lililobaki lina dhamana kwa mujibu wa sheria.



Lwakatare sasa amebaki na shtaka moja tu la kula njama za kutaka kumdhuru kwa sumu Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications, Denis Msacky. Kesi hiyo itatajwa kesho katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.


chanzo: tanzania daima