Kambi ya Upinzani Bungeni imetoa tuhuma nzito kwa
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ikidai kuwa anajihusisha na
mtandao wa ujangili nchini. Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk
Emmanuel Nchimbi amejibu tuhuma hiyo akisema ni za uongo huku akiituhumu
kambi hiyo kuwa imedanganya wakati inajua ukweli kuhusu tuhuma dhidi ya
Kinana. Akiwasilisha maoni ya upinzani kuhusu Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka 2013/14, Msemaji wa
Kambi ya Upinzani kuhusu Maliasili, Mchungaji Peter Msigwa alisema
vitendo vya ujangili vimekuwa vikilitia doa taifa kwenye jumuiya za
kimataifa. “Kwa bahati mbaya ni kwamba wahusika wengi ambao wanatajwa
kwa ushahidi ni makada maarufu na wengine ni viongozi waandamizi wa
CCM,” alisema Mchungaji Msigwa. “Tumeshuhudia watuhumiwa wengine wa
ujangili ambao Ikulu imediriki kuwapatia nafasi kubwa za uongozi wa
taifa hili, licha ya kutajwa kwenye ripoti ya uchunguzi kuhusiana na
ujangili.” Alisema mwaka 2009, meli ya Kampuni ya Wakala wa Meli ya
Sharaf Shipping inayomilikiwa na Kinana ilikamatwa China ikiwa na
makontena yenye nyara za Serikali ikiyasafirisha kwenda Hong Kong. “Nyaraka
zilizopo Ofisi za Wakala wa Usajili wa Kampuni na Biashara (Brela),
zinaonyesha kuwa kampuni hiyo ya Kinana ilisajiliwa Oktoba 2003 na
kupewa hati na. 47221. “Nyaraka zinaonyesha kuwa Kinana anamiliki
hisa 7,500 kati ya 10,000 za kampuni hiyo iliyosajiliwa Dar es Salaam.
Mshirika mwenzake katika kampuni hiyo, Rahma Hussein ambaye ni mke wake
anamiliki hisa 2,500,” alisema Msigwa. |
No comments:
Post a Comment